Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) limesema limepokea
kwa masikitiko taarifa za kufukuzwa kwa waandishi wa habari wa kituo cha
Televisheni cha shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) wakati wakitekeleza
wajibu wao katika ofisi za Chadema.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga amesema katika
taarifa kwa vyombo vya habari jana kuwa waandishi wa TBC walikwenda kuchukua
habari wakijumuika na wenzao wa vyombo vingine, lakini walibaguliwa na kunyimwa
haki ya kupata habari.
“Kitendo cha kuwafukuza waandishi hao waliokwenda
kwenye mkutano huo uliomhusisha nwanasheria wa chama hicho,Tundu Lissu
hakikubaliki kwa kuwa ni ubaguzi ambao mbali na kuwanyima wananchi wanaotazama
TBC haki ya kupata habari,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema vitendo vya kuwabughudhi
waandishi wa habari havipaswi kupewa nafasi katika nchi kwa kuwa vinawanyima
wananchi haki ya kupata taarifa kama ilivyoainishwa kwemye ibara ya 18(d) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo inasema TEF haitavumilia watu au
taasisi yoyote iwe binafsi au ya umma ambayo itaingilia uhuru wa habari au
kuwakwaza waandishi katika kutekeleza wajibu wao.
Source:Mwananchi Newspaper

No comments:
Post a Comment