Monday, 31 July 2017

MAHUSIANO

DALILI ZINAZOONESHA KUWA UPO KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI AMBAYO SIO SAHIHI 

Sisi sote tunapenda kuwa na furaha pamoja na kupendwa  katika mahusiano yetu ya kimapenzi. Lakini wakati mwingine, huwa kuna dalili ambazo hazifai katika mahusiano yetu, na ni vema kuzingatia dalili hizi. Zifuatazo ni baadhi ya dalili au ishara kwamba upo katika mahusiano ambayo sio sahihi

1.KUKOSA KUAMINIANA
Kumuamini mpenzi wako ni jambo la msingi sana katika mahusiano yoyote yale.Unapaswa kumuamini mpenzi wako katika kila jambo ambalo analifanya, lakini kama upo katika mahusiano ambayo unaona humuamini mwenza wako, basi ujue mahusiano yenu ni ya kutilia shaka.

2. KUKUDHARAU MARA KWA MARA

Dharau ni jambo baya sana kutokea katika mahusiano. Mwenza wako anapaswa kukufanya wewe ujione kuwa ni bora, na sio kukudharau. Kama mwenza wako anakudharau, fahamu kuwa mahusiano yenu yapo katika hali ya hatari, hivyo unapaswa kuwa makini.

3.KUKOSEKANA KWA MAWASILIANO
Katika mahusiano, mawasiliano ni jambo la muhimu sana. Hauwezi kukaa kwa muda mrefu bila hata kuwasiliana na mwenza wako kwa sababu wapenzi wanahitaji kushirikishana katika mambo mbalimbali. Kama ukiona mawasiliano yenu ni ya kusuasua ujue kuwa unapaswa kuuangalia uhusiano kwa jicho la ukaribu zaidi.

4.KUKOSEANA HESHIMA
Hii ni dalili kubwa inayoonesha kuwa mahusiano uliyonayo hayafai. Kama unaona kuwa mwenza wako mara nyingi hatimizi ahadi zake, hakupi heshima ile ambayo wewe unapaswa kupewa au anakufanya ujione kuwa wewe sio wa muhimu, basi ujue mahusiano kama hayo sio mazuri sana wewe kuendelea kuwepo.
Tafakari upya.

5. HASIRA ZISIZO NA MAANA
Kama unaona mwenza wako hapendi kazi yako, hafurahii mafanikio yako au anachukia wewe kuwa na marafiki wengi, basi ujue kuwa huo uhusiano haufai. Mpenzi wako anapaswa kuwa mtu ambaye anafurahia mafanikio yako  na sio kuwa mshindani wako.

6. KUJARIBU KUKUTAWALA
Sisi sote tunakubali kuwa tunaweza kwenda kwa wapenzi wetu na kuomba ushauri. Lakini kama unaona kuwa mwenza wako anakushauri au anakulazimisha kufanya jambo fulani mara kwa mara, hiyo inaweza kuwa ni njia mojawapo ya kutaka kukutawala. Kwa mfano, anakuchagulia marafiki, anakuchagulia kitu cha kufanya ukiwa hauna kazi, anakupangia muda wa kuwa na familia na marafiki. Ukiona jambo kama hilo, ni muhimu ukajaribu kuangalia kwa umakini sana.

7.UNATUMIA  NGUVU KUBWA KUMTETEA MPENZI WAKO
Sio kila mtu atampenda mwenza wako kama ambavyo wewe mwenyewe unampenda. Lakini unapaswa kuwa na wasiwasi endapo utaona kuwa ndugu zako wote pamopja namarafiki zako wanakuwa hawana imani na mahusiano yenu. Hivyo, unapaswa kuutazama upya uhusiano huo.

8.KUJITENGA NA JAMII
Kama unajikuta unajitenga na jamii kwa sababu ya mahusiano, fahamu kuwa hiyo ni dalili nyingine inayoonesha kuwa upo katika mahusiano yasiyofaa. Kumbuka kuwa unahitaji kuwa pamoja na ndugu na marafiki pia. Kama mpenzi wako anataka muda wote uwe naye yeye tu, hataki uwe na marafiki au familia yako, ujue kuwa b unapaswa kuwa makini sana.

9.KUFICHIANA SIRI
Unapokuwa katika mahusiano, hauna sababu ya kuficha siri. Kama unaona kuwa mwenza wako anaweza kuja kutumia taarifa zako dhidi yako, unapaswa kutambua kuwa mahusiano hayo hayafai. Wenza wanapaswa kuzungumza kwa uwazi bila siri yoyote.

10.KUBADILIKA ILI UWEZE KUMFURAHISHA MWENZA WAKO
Endapo unajikuta unalazimika kubadilika ili tu uweze kumfurahisha mpenzi wako, tambua kuwa mahusiano ya namna hiyo hayafai. Kama unajikuta unalazimika kubadili namna unavyovaa, unavyozungumza ili tu uweze kumfurahisha mwenza wako, fahamu kuwa inabidi uutazame upya uhusiano huo.

11. KUGOMBANA MARA KWA MARA
Katika mahusiano, kutofautiana ni jambo la kawaida sana. Lakini kama unajikuta unagombana na mpenzi wako kila siku kwa ajili ya vitu vidogo vidogo tu, fahamu kuwa huo unaweza usiwe uhusiano mwema wa wewe kuendelea kuwepo.

12. KULALAMIKA KILA SIKU
Kama kila siku unakuta mpenzi wako anakulalamikia kwa kila kitu au anatafuta namna ya kukulalamikia. fahamu kuwa hiyo ni dalili isiyofaa katika mahusiano. Hutakiwi kumlaumu mpenzi wako kwa kila kitu.

13. ANAWAZA NGONO TU MUDA WOTE
Ngono ni sehemu tu ya mapenzi, lakini sio ndiyo kila kitu katika mapenzi. Kama unakuta unawasiliana na mwenza wako mara chache sana, na muda ambao mnakuwa karibu ni ule tu ambao mnakuwa wote kitandani, fahamu kuwa unapaswa kuwa makini sana na uhusiano wa aina hiyo.

14. MMOJA WENU ANA NGUVU KULIKO MWINGINE
Katika mahusiano, haipaswi mmojawapo akawa na nguvu kuliko mwingine, na badala yake kila mmoja awe sawa na mwingine. Kama mmoja wenu anakuwa na nguvu kuliko mwingine, kwa mfano, yeye ndo ankuwa muamuzi katika kila kitu, fahamu kuwa uhusiano wenu una matatizo mahali.

15.UNAPENDA TU KUWA KATIKA MAHUSIANO, LAKINI HAUFURAHII
Kuna watu unakuta anapenda tu kuwa katika mahusiano, lakini hafurahii mahusiano hayo. Ameamua kuwa katika mahusiano ili tu asiwe mpweke, na sio kwamba anafurahia uhusiano aliopo. Ukijiona hufurahii kuwa katika mahusiano, fahamu kuwa sio vema sana wewe kuwepo katika hayo mahusiano.


Kwa ujumla, kuwa na dalili kama hizo katika mahusiano yako, haimanishi kuwa mahusiano yako hayawezi kuwa mazuri. Na ili mahusiano yenu yaondokane na dalili hizo hapo juu, itategemea na juhudi zenu wawili katika kuuimarisha uhusiano wenu.

No comments:

Post a Comment

MAHUSIANO

DALILI ZINAZOONESHA KUWA UPO KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI AMBAYO SIO SAHIHI  Sisi sote tunapenda kuwa na furaha pamoja na kupendwa  katik...