Friday, 28 July 2017

MUDA NI MALI, KIVIPI MUDA WAKO UNA THAMANI?


Muda ni umbali wa kifikra uliopo kati ya matukio mawili yanayofuatana. Umbali huu huweza kupimwa kwa kutumia kizio cha sekunde, dakika, au saa.
Sekunde 60 hutengeneza dakika moja; dakika 60 saa moja; masaa 24 siku moja; siku saba wiki moja; wiki 4 mwezi mmoja; miezi 12 mwaka mmoja. Na kwa ujumla, kuna dakika 60 katika saa; dakika 1,440 katika siku; dakika 10,080 katika wiki; dakika 40,320 katika mwezi; na dakika 483,840 katika mwaka.
Na kwa kweli, muda ni mali inayopatikana kwa usawa kwa kila mtu ili aitumie katika kutekeleza majukumu yake.
Kama hivyo ndivyo, kwa nini baadhi ya watu wanakuwa wanaweza kukamilisha kazi zao kwa wakati kuliko watu wengne?
Jibu linakuja kwenye namna ambavyo kila mmoja wetu anaweza kupanga bajeti ya muda na kuheshimu ratiba hiyo wakati wa kutumia muda tulio nao.
Utafiti unaonesha kuwa watu wengi wanaofanikiwa katika  mambo yao ni wale ambao wanatumia muda wao vizuri.

Faida za kutunza muda vizuri
Zifuatazo ni faida mbalimbali ambazo unaweza kuzipata endapo utakuwa na menejimenti nzuri ya muda

Unakuwa mzalishaji bora, lakini pia itakusaidia kufanya mambo yako kwa ufanisi  wa hali ya juu. Hii inatokana na ukweli ya kwamba menejimenti nzuri ya muda inakusaidia kuwa makini na kuzingatia kile ambacho unakifanya kwa wakati husika.

Unakuwa na sifa njema katika kazi yako. Unapokuwa makini na kufanya kazi kwa ufanisi, itapelekea sifa njema kwako kutokana na ufanisi ulionao katika kazi yako. Ufanisi ambao unatokana na wewe kuwa na menejimenti nzuri ya muda.

Itakusaidia kupunguza msongo wa mawazo. Hii ni kwa sababu menejimenti nzuri ya muda itakusaidia katika kukamilisha kila jambo kwa wakati husika hivyo kukuondolea wasiwasi na mawzo katika akili yako.

Itakusaidia katika kupiga hatua kimaendeleo. Hii ni kwa sababu menejimenti ya muda itakusaidia kuzingatia kufanya vitu vya msingi na ambavyo vinaweza kukusaidia katika kupiga hatua kimaendeleo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Pia unakuwa na nafasi nzuri ya kufikia malengo yako ya kimaisha. Hii ni kwa sababu menejimenti nzuri ya muda inakusaidia katika kufanya vitu kwa wakati, kwa umakini na ufanisi wa hali ya juu. Pia inakusaidia katika kutekeleza vipaumbele ulivyonavyo katika kufikia malengo yako ya kimaisha.

Hasara za kushindwa kutunza muda vizuri

Kushindwa kusimamia muda wako vizuri kutapelekea faida zilizotajwa hapo juu kugeuka na kuwa hasara.
Kwa mfano, kutakuwa na kukosekana kwa ufanisi katika kazi unayoifanya kutokana na ukweli kwamba ,unakosa umakini katika kile ambacho unakuwa unakifanya.
Pia itakupelekea kuwa na msongo mkubwa wa mawazo kwa sababu unakuwa unashindwa kukamilisha mambo yako kwa wakati unaotakiwa.

Mbinu za kutunza muda

Zifuatazo ni mbinu mbalimbali ambazo zitakusaidia katika kutumia muda wako vizuri.

Jiwekee malengo yako. Tafiti zinaonesha kwamba wale watu ambao wanajiwekea malengo wanakuwa na uwezo wa kuona ni kwa kiasi gani wametimiza kile ambacho walikidhamiria kukitimiza kuliko wale ambao hawana malengo.

Weka  vipaumbele vyako. Unaweza ukawa na vitu vingi sana vya kufanya kwa wakati mmoja, lakini unatakiwa kuzingatia kipaumbele chako katika hayo yote ni kipi hasa na kisha uanze na hiko.
Kwa mfano, unaweza ukawa unataka kusoma na kulala kwa wakati mmoja. Lakini unachotakiwa kufanya ni kuangalia ni kipi kati ya hivyo viwili ni kipaumbele chako wewe na kisha uanze nacho.
Hakikisha matendo yako yanaendana na kipaumbele chako. Kwa mfano, kipaumbele chako kilikuwa ni kutumia masaa mawili kwa ajili ya kusoma. Lakini wakati unasoma unaanza kutumia simu kwa kusoma ujumbe mbalimbali ambazo umetumiwa na hata kuzijibu, kitu ambacho kitakufanya upoteze muda wako na hata kupoteza umakini katika kusoma kwako.

Jifunze kusema hapana. Jifunze kukataa kufanya jambo ambalo unaona halina thamani yoyote katika maisha yako na wala haliendani na vipaumbele ulivyonavyo. Jifunze kukubali kufanya jambo ambalo lina thamani katika maisha yako kwa mfano, kufanya mazoezi, kukaa na familia yako, kupumzika na mengineyo yanayofanana na hayo.

Epuka kufanya vitu ambavyo vinakupotezea muda wako. Tambua vitu ambavyo vinakufanya upoteze muda kama vile meseji, mitandao ya kijamii, watu na vitu vingine. Ukishavigundua unatakiwa kuviondoa, usiruhusu muingiliano wa kitu chochote kile katika muda ambao unatakiwa kuzingatia jambo fulani.
Lakini pia jambo lingine ambalo linaweza kukufanya wewe upoteze muda ni pamoja na kuwa na mtazamo hasi katika jambo fulani. Hii ni kwa sababu unapokuwa na mtazamo hasi katika jambo fulani, utakuwa unakosa umakini katika jambo hilo na hivyo kukupotezea tu muda.
Usipoteze muda wako kulalamika kuhusu makosa ambayo umeshawahi kuyafanya hapo nyuma. Cha msingi unachotakiwa kukifanya ni kujifunza kutokana na makosa na kusonga mbele.
Usipoteze muda wako kujilaumu kuhusu makosa ambayo ulishayafanya kipindi cha nyuma, badala yake songa mbele.
Epuka kuwa na udhuru. Imezoeleka kuwa watu wengi hawapendi kufanya kazi mbalimbali ambazo huwa hawazipendi. Suluhisho pekee katika hili ni kufanya tu hizo kazi kwanza ili kuweza kuokoa muda.
Acha tabia za kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja. Unatakiwa kufanya jambo moja kwa wakati mmoja kwani kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kunaweza kukakupotezea muda wako.
Tafiti zinaonesha kuwa watu ambao wanadhani wanaokoa muda kwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja wanaweza wasikamilishe kwa haraka au kwa umakini kama ambavyo wangefanya kila jambo kwa wakati mmoja.
Kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja kunapunguza nguvu ya ubongo katika kufikiria lakini pia kunaleta msongo wa mawazo jambo ambalo linaathiri kumbukumbu katika ubongo. Wakati mwingine kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja ni jambo lisiloweza kuepukika, lakini hautakiwi kufanya hivyo kwa siku nzima.
Kama utazingatia jambo moja kwa wakati mmoja, utakuwa makini katika kile ambacho unakifanya  kwa wakati unaotakiwa.
Vilevile ukifanya jambo moja kwa wakati mmoja na kulimaliza kabla hujaenda kufanya jambo lingine, utajikuta unatumia muda mchache zaidi kulimaliza. Hii itakusaidia wewe kupata muda  zaidi wa kufanya kitu kingine ambacho ulipanga kukifanya.  
Hitimisho
Kwa ujumla, muda ni rasilimali ambayo inamilikiwa na kila mtu. Sote ni matajiri wa muda. Changamoto imo katika namna tunavyoutumia muda muda huo. Chunga muda wako.


No comments:

Post a Comment

MAHUSIANO

DALILI ZINAZOONESHA KUWA UPO KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI AMBAYO SIO SAHIHI  Sisi sote tunapenda kuwa na furaha pamoja na kupendwa  katik...