Monday, 31 July 2017

MAHUSIANO

DALILI ZINAZOONESHA KUWA UPO KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI AMBAYO SIO SAHIHI 

Sisi sote tunapenda kuwa na furaha pamoja na kupendwa  katika mahusiano yetu ya kimapenzi. Lakini wakati mwingine, huwa kuna dalili ambazo hazifai katika mahusiano yetu, na ni vema kuzingatia dalili hizi. Zifuatazo ni baadhi ya dalili au ishara kwamba upo katika mahusiano ambayo sio sahihi

1.KUKOSA KUAMINIANA
Kumuamini mpenzi wako ni jambo la msingi sana katika mahusiano yoyote yale.Unapaswa kumuamini mpenzi wako katika kila jambo ambalo analifanya, lakini kama upo katika mahusiano ambayo unaona humuamini mwenza wako, basi ujue mahusiano yenu ni ya kutilia shaka.

2. KUKUDHARAU MARA KWA MARA

Dharau ni jambo baya sana kutokea katika mahusiano. Mwenza wako anapaswa kukufanya wewe ujione kuwa ni bora, na sio kukudharau. Kama mwenza wako anakudharau, fahamu kuwa mahusiano yenu yapo katika hali ya hatari, hivyo unapaswa kuwa makini.

3.KUKOSEKANA KWA MAWASILIANO
Katika mahusiano, mawasiliano ni jambo la muhimu sana. Hauwezi kukaa kwa muda mrefu bila hata kuwasiliana na mwenza wako kwa sababu wapenzi wanahitaji kushirikishana katika mambo mbalimbali. Kama ukiona mawasiliano yenu ni ya kusuasua ujue kuwa unapaswa kuuangalia uhusiano kwa jicho la ukaribu zaidi.

4.KUKOSEANA HESHIMA
Hii ni dalili kubwa inayoonesha kuwa mahusiano uliyonayo hayafai. Kama unaona kuwa mwenza wako mara nyingi hatimizi ahadi zake, hakupi heshima ile ambayo wewe unapaswa kupewa au anakufanya ujione kuwa wewe sio wa muhimu, basi ujue mahusiano kama hayo sio mazuri sana wewe kuendelea kuwepo.
Tafakari upya.

5. HASIRA ZISIZO NA MAANA
Kama unaona mwenza wako hapendi kazi yako, hafurahii mafanikio yako au anachukia wewe kuwa na marafiki wengi, basi ujue kuwa huo uhusiano haufai. Mpenzi wako anapaswa kuwa mtu ambaye anafurahia mafanikio yako  na sio kuwa mshindani wako.

6. KUJARIBU KUKUTAWALA
Sisi sote tunakubali kuwa tunaweza kwenda kwa wapenzi wetu na kuomba ushauri. Lakini kama unaona kuwa mwenza wako anakushauri au anakulazimisha kufanya jambo fulani mara kwa mara, hiyo inaweza kuwa ni njia mojawapo ya kutaka kukutawala. Kwa mfano, anakuchagulia marafiki, anakuchagulia kitu cha kufanya ukiwa hauna kazi, anakupangia muda wa kuwa na familia na marafiki. Ukiona jambo kama hilo, ni muhimu ukajaribu kuangalia kwa umakini sana.

7.UNATUMIA  NGUVU KUBWA KUMTETEA MPENZI WAKO
Sio kila mtu atampenda mwenza wako kama ambavyo wewe mwenyewe unampenda. Lakini unapaswa kuwa na wasiwasi endapo utaona kuwa ndugu zako wote pamopja namarafiki zako wanakuwa hawana imani na mahusiano yenu. Hivyo, unapaswa kuutazama upya uhusiano huo.

8.KUJITENGA NA JAMII
Kama unajikuta unajitenga na jamii kwa sababu ya mahusiano, fahamu kuwa hiyo ni dalili nyingine inayoonesha kuwa upo katika mahusiano yasiyofaa. Kumbuka kuwa unahitaji kuwa pamoja na ndugu na marafiki pia. Kama mpenzi wako anataka muda wote uwe naye yeye tu, hataki uwe na marafiki au familia yako, ujue kuwa b unapaswa kuwa makini sana.

9.KUFICHIANA SIRI
Unapokuwa katika mahusiano, hauna sababu ya kuficha siri. Kama unaona kuwa mwenza wako anaweza kuja kutumia taarifa zako dhidi yako, unapaswa kutambua kuwa mahusiano hayo hayafai. Wenza wanapaswa kuzungumza kwa uwazi bila siri yoyote.

10.KUBADILIKA ILI UWEZE KUMFURAHISHA MWENZA WAKO
Endapo unajikuta unalazimika kubadilika ili tu uweze kumfurahisha mpenzi wako, tambua kuwa mahusiano ya namna hiyo hayafai. Kama unajikuta unalazimika kubadili namna unavyovaa, unavyozungumza ili tu uweze kumfurahisha mwenza wako, fahamu kuwa inabidi uutazame upya uhusiano huo.

11. KUGOMBANA MARA KWA MARA
Katika mahusiano, kutofautiana ni jambo la kawaida sana. Lakini kama unajikuta unagombana na mpenzi wako kila siku kwa ajili ya vitu vidogo vidogo tu, fahamu kuwa huo unaweza usiwe uhusiano mwema wa wewe kuendelea kuwepo.

12. KULALAMIKA KILA SIKU
Kama kila siku unakuta mpenzi wako anakulalamikia kwa kila kitu au anatafuta namna ya kukulalamikia. fahamu kuwa hiyo ni dalili isiyofaa katika mahusiano. Hutakiwi kumlaumu mpenzi wako kwa kila kitu.

13. ANAWAZA NGONO TU MUDA WOTE
Ngono ni sehemu tu ya mapenzi, lakini sio ndiyo kila kitu katika mapenzi. Kama unakuta unawasiliana na mwenza wako mara chache sana, na muda ambao mnakuwa karibu ni ule tu ambao mnakuwa wote kitandani, fahamu kuwa unapaswa kuwa makini sana na uhusiano wa aina hiyo.

14. MMOJA WENU ANA NGUVU KULIKO MWINGINE
Katika mahusiano, haipaswi mmojawapo akawa na nguvu kuliko mwingine, na badala yake kila mmoja awe sawa na mwingine. Kama mmoja wenu anakuwa na nguvu kuliko mwingine, kwa mfano, yeye ndo ankuwa muamuzi katika kila kitu, fahamu kuwa uhusiano wenu una matatizo mahali.

15.UNAPENDA TU KUWA KATIKA MAHUSIANO, LAKINI HAUFURAHII
Kuna watu unakuta anapenda tu kuwa katika mahusiano, lakini hafurahii mahusiano hayo. Ameamua kuwa katika mahusiano ili tu asiwe mpweke, na sio kwamba anafurahia uhusiano aliopo. Ukijiona hufurahii kuwa katika mahusiano, fahamu kuwa sio vema sana wewe kuwepo katika hayo mahusiano.


Kwa ujumla, kuwa na dalili kama hizo katika mahusiano yako, haimanishi kuwa mahusiano yako hayawezi kuwa mazuri. Na ili mahusiano yenu yaondokane na dalili hizo hapo juu, itategemea na juhudi zenu wawili katika kuuimarisha uhusiano wenu.

Saturday, 29 July 2017

CHADEMA YAJIBU TUHUMA ZA TEF

Kuhusu Mwandishi wa TBC kuzongwa/kuzuiliwa kutimiza wajibu wake

Tumepokea kupitia vyombo vya Habari taarifa za tukio la Mwandishi wa habari wa TBC kushindwa kutimiza wajibu wake katika makao makuu ya CHADEMA.
Tunapenda kuweka wazi kuwa tukio hili halikufanywa kwa maelekezo ya kiongozi yeyote na kama Chama htatujawahi na hatuna sera wala msimamo wa kubagua chombo chochote cha habari.
Kwa hatua za awali, tunafanyia uchumguzi tukio hilo ili kuweza kubainisha nini hasa kilitokea katika siku hiyo na tunategemea kupata ushirikiano kutoka kwa mwandishi husika katika uchunguzi wetu.
Tunapenda kuwahakikishia waandishi wote wa habari kuwa wataendelea kuwa salama katika matukio yote ambayo yatakuwa yakifanywa na CHADEMA na watapata ushirikiano unaostahili.
Baada ya uchunguzi wetu kukamilika tutatoa taarifa kamili juu ya tutakachokuwa tumebaini na hatua tutakazozichukua.
Sisi tunaamini katika uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa waandishi na haki ya kupata na kutoa habari/taarifa kuwa nguzo kuu katika kujenga taifa la demokrasia na hatimayea kufikia maendeleo ya kweli.
Imani yetu hiyo tumekuwa tukiidhihirisha kwa vitendo hadharani, mfano CHADEMA ni taasisi ya kwanza ya kisiasa iliyotia saini na kukubaliana na Azimio la Dar es salaam juu ya uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji (hatuna uhakika kama ipo nyingine iliyofanya hivyo hadi sasa).
Tunapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia wadau wote wa habari wakiwemo waandishi, wahariri na wananchi kuwa tutaendelea kuionesha imani hiyo kwa vitendo katika shughuli zetu zote za kisiasa .

John Mrema,Mkurugenzi wa Itifaki,Mawasiliano na Mambo ya nje-CHADEMA


source:Jamii forum

TEF yalaani kufukuzwa kwa waandishi wa habari mkutano wa chadema


Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) limesema limepokea kwa masikitiko taarifa za kufukuzwa kwa waandishi wa habari wa kituo cha Televisheni cha shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) wakati wakitekeleza wajibu wao katika ofisi za Chadema.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari jana kuwa waandishi wa TBC walikwenda kuchukua habari wakijumuika na wenzao wa vyombo vingine, lakini walibaguliwa na kunyimwa haki ya kupata habari.
“Kitendo cha kuwafukuza waandishi hao waliokwenda kwenye mkutano huo uliomhusisha nwanasheria wa chama hicho,Tundu Lissu hakikubaliki kwa kuwa ni ubaguzi ambao mbali na kuwanyima wananchi wanaotazama TBC haki ya kupata habari,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema vitendo vya kuwabughudhi waandishi wa habari havipaswi kupewa nafasi katika nchi kwa kuwa vinawanyima wananchi haki ya kupata taarifa kama ilivyoainishwa kwemye ibara ya 18(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo inasema TEF haitavumilia watu au taasisi yoyote iwe binafsi au ya umma ambayo itaingilia uhuru wa habari au kuwakwaza waandishi katika kutekeleza wajibu wao.

Source:Mwananchi Newspaper

Friday, 28 July 2017

MAHUSIANO



FAHAMU MBINU MBALIMBALI AMBAZO ZITAKUSAIDIA KUDUMU 
KATIKA MAHUSIANO YAKO
Mahusiano ni jambo la muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku. Ni muhimu kwa ajili ya furaha, lakini pia ni muhimu kwa ajili ya maendeleo yetu. Lakini bado, utafiti unaonesha kwamba zaidi ya asilimia 40 ya ndoa zinaishia kwenye kupeana talaka. Huu ni uthibitisho wa kwamba, mahusiano si jambo rahisi.

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kukusaidia kudumu katika mahusiano

1.KUJIFAHAMU VIZURI
Kabla ya kuingia katika mahusiano, unapaswa kwanza ujifahamu wewe ni nani ukiwa peke yako, wewe ni nani ukiwa katika mahusiano, na wewe ni nani ukiwa na watu wengine kwa ujumla. Vile vile unapaswa kufahamu unahitaji nini na ni nini matarajio yako katika mahusiano
2.KUMUAMINI MWENZAKO
Mojawapo kati ya mambo ya msingi sana katika mahusiano ni pamoja na kuaminiana. Unapaswa kumuamini mwenza wako kwani bila kumuamini, hakuna jambo lolote ambalo linaweza kufanyika. Na kama humuamini mwenzako, basi mbinu zote ambazo zinafuata hapo chini zitakuwa hazina umuhimu wowote ule kwako na katika mahusiano yako.
3.MKUBALI  MWENZA WAKO
Unapokuwa katika mahusiano, unapaswa kumkubali mwenza wake vile namna alivyo, kwa mfano, anavyoonekana na kitu anachokifanya , na kama ana madhaifu kadhaa ambayo yanaweza kurekebishika, mnaweza kusaidia kuyarekebisha kwa pamoja. Na pia kama  kuna tofauti kadhaa baina yenu, kila mmoja wenu hana budi kuziheshimu hizo tofauti kwani sio rahisi mkafanana kwa kila kitu.

4.MFAHAMIANE VIZURI
Wenza wanapaswa kufahamiana vizuri na kwa undani zaidi. Unapaswa kufahamu familia ya mwenza wako, asili yao, kufahamu tabia yake, kufahamu vitu ambavyo mwenzako anavipenda na ambavyo havipendi. Hii itakusaidia kujua namna ya kuishi nae vizuri ili muweze kuenda sawa na kudumu katika mahusiano yenu.
5.KUWA NA MAWASILIANO YA MARA KWA MARA
Ni vema ukajiwekea tabia ya kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na mwenza wako na ukawa unamjibu simu na meseji zake kwa wakati. Lakini pia mnaweza kuwa mnawasiliana kupitia hata mitandao ya kijamii kama inawezekana.
6.NAMNA AMBAVYO WEWE NA MWENZA WAKO MNASULUHISHA MATATIZO KATIKA MAHUSIANO YENU
Kwanza unapaswa kufahamu kuwa katika mahusiano, kutofautiana ni jambo la kawaida sana. Usitarajie kuwa na furaha siku zote, badala yake unapaswa kufahamu kuwa kuna huzuni pia. Wapenzi wanaodumu, hata wakiwa na hasira, hutafuta namna ya kuwa karibu, na wakishatatua tatizo, wanasamehe na kusahau kwani hata  Utafiti unaonesha kuwa, wapenzi wanaosuluhisha matatizo yao na kusahau, huwa wanadumu.Na jambo la msingi zaidi ni kwamba, huwa wanajifunza kupitia zile tofauti ambazo zinatokea baina yao, jambo ambalo husaidia mahusiano yao kudumu kwa muda mrefu.
7.NAMNA AMBAVYO MNASAIDIANA KATIKA MATATIZO MBALIMBALI
Moja kati ya mambo ya kudumisha mahusiano, ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuwa pamoja katika matatizo mbalimbali. Unapaswa kujiuliza, Je, matatizo yako yanakuleta wewe na mwenza wako pamoja au yanawatenganisha? Mnashirikiana katika matatizo au manashirikiana katika furaha peke yake?Utafiti unaonesha kuwa wapenzi ambao wanashirikiana katika matatizo, wanajenga muunganiko mzuri ambao unaweza kudumu.
8.KUWA NA MALENGO YA PAMOJA
Mkiwa kama wapenzi ambao mnataka kudumu, mnapaswa kuwa na malengo ya pamoja katika maisha yenu. Mnatakiwa kuishi mkiwa kama “team”, jambo ambalo litawasaidia katika kufikia malengo ambayo mnakuwa mmejiwekea kwa pamoja.Lakini mnapaswa kukumbuka kuwa mnapaswa kujiwekea malengo ambayo yatawasaidia nyinyi wote wawili. Hii itawasaidia sana kutokana na ukweli kwamba itawahakikishia kuwa mnakuwa na “uelekeo unaofanana” na hata mwisho wa siku mnaweza kuja kusheherekea kwa pamoja mafanikio ambayo mnakuwa mmeyapata.Uchunguzi unaonesha kuwa moja kati ya vitu muhimu kwa ajili ya furaha ni kupambana kutimiza malengo ambayo ni muhimu. Na kwa upande mwingine, moja kati ya vitu muhimu kwa ajili ya kuwa na mahusiano yenye furaha ni pamoja na kuwa na malengo ambayo mtajaribu kuyafikia kwa pamoja.
 9.KUWA MKWELI NA MUWAZI
Unapaswa kuwa mkweli na muwazi kwa mwenza wako kueleza namna ambavyo unajisikia au una wasiwasi  au kitu ambacho unakihitaji.
10.KUPEANA “ SUPPORT”
Kuna namna mbalimbali ambazo wapenzi wanaweza wakapeana support. Kwa mfano, kupeana support za kihisia kama vile kumsikiliza mweza wako kama anahitaji kuzungumza na wewe, au ana mawazo au pengine anahitaji ushauri n.k Pia kumpa ushirikiano wa aina yoyote ambao anakuwa anauhitaji kutoka kwako, kumpatia taarifa kuhusu mambo mbalimbali kama atakuwa anahitaji na kadhalika.
11.KUWA NA FIKRA CHANYA
Tafiti zinaonesha kuwa mara nyingi Wapenzi wanaodumu katika mahusiano yao huwa wanazingatia katika mambo mazuri yaliyopo katika mahusiano yao kuliko yale mabaya. Na pia huwa hawawazi mabaya juu ya mahusiano yao.
12.KUTOKU”PRETEND”
Wapenzi wanaodumu huwa hawa “pretend” katika mahusiano yao, na badala yake wanakuwa wakweli. Ukizoea kupretend katika mahusiano yako, basi utashindwa kudumu kwani utajikuta unashindwa kuendelea kuwepo katika mahusiano hayo baada ya muda fulani.
13.KUMTETEA  MWENZA WAKO
Unapaswa kumlinda mwenza wako dhidi ya mtu au watu wengine. Kwa mfano, ukimsikia mtu yoyote anaongea neno baya dhidi ya mwenza wako unapaswa kumtetea mwenza.Hii ni kutokana na ukweli kwamba, aibu ya mwenza wako ni aibu yako pia, hivyo hauna budi kumtetea kwa namna yoyote ile.
14.KUMFANYIA SURPRISE PAMOJA NA KUMFANYIA VITU AMBAVYO YEYE ANAVIPENDA
Unapaswa kumfanyia surprise mwenza wako hata kama ni mara moja moja  au hata kama zikiwa ni surprise ndogondogo, na pia kumfanyia vitu ambavyo yeye anavipenda sana. Hii itamfanya awe na furaha wakati wote
15.KUTENGA MUDA WA KUWA PAMOJA
Wenza wanapaswa kutenga muda wa kuwa pamoja na kufurahi pamoja. Kwa mfano, mnaweza mkatenga muda wa kwenda  kupata pamoja chakula cha usiku, kuweka muda wa kutoka out na kadhalika.

16.wenza wanapokuwa pamoja, hawana budi kuwa wanashikana mikono, wanakumbatiana, kupigana mabusu, kushikana mabega na mengine kama hayo. Kitaalamu, hii inasaidia sana katika kupunguza msongo wa mawazo, kuongeza hamasa, na kupunguza presha.


Kimsingi, mahusiano yenye furaha na yanayodumu huwa hayatokei tu kutoka sehemu fulani, na badala yake huwa yanatengenezwa. Lakini pia, mahusiano yenye furaha  ni muhimu kwa ajili ya maisha yetu

MUDA NI MALI, KIVIPI MUDA WAKO UNA THAMANI?


Muda ni umbali wa kifikra uliopo kati ya matukio mawili yanayofuatana. Umbali huu huweza kupimwa kwa kutumia kizio cha sekunde, dakika, au saa.
Sekunde 60 hutengeneza dakika moja; dakika 60 saa moja; masaa 24 siku moja; siku saba wiki moja; wiki 4 mwezi mmoja; miezi 12 mwaka mmoja. Na kwa ujumla, kuna dakika 60 katika saa; dakika 1,440 katika siku; dakika 10,080 katika wiki; dakika 40,320 katika mwezi; na dakika 483,840 katika mwaka.
Na kwa kweli, muda ni mali inayopatikana kwa usawa kwa kila mtu ili aitumie katika kutekeleza majukumu yake.
Kama hivyo ndivyo, kwa nini baadhi ya watu wanakuwa wanaweza kukamilisha kazi zao kwa wakati kuliko watu wengne?
Jibu linakuja kwenye namna ambavyo kila mmoja wetu anaweza kupanga bajeti ya muda na kuheshimu ratiba hiyo wakati wa kutumia muda tulio nao.
Utafiti unaonesha kuwa watu wengi wanaofanikiwa katika  mambo yao ni wale ambao wanatumia muda wao vizuri.

Faida za kutunza muda vizuri
Zifuatazo ni faida mbalimbali ambazo unaweza kuzipata endapo utakuwa na menejimenti nzuri ya muda

Unakuwa mzalishaji bora, lakini pia itakusaidia kufanya mambo yako kwa ufanisi  wa hali ya juu. Hii inatokana na ukweli ya kwamba menejimenti nzuri ya muda inakusaidia kuwa makini na kuzingatia kile ambacho unakifanya kwa wakati husika.

Unakuwa na sifa njema katika kazi yako. Unapokuwa makini na kufanya kazi kwa ufanisi, itapelekea sifa njema kwako kutokana na ufanisi ulionao katika kazi yako. Ufanisi ambao unatokana na wewe kuwa na menejimenti nzuri ya muda.

Itakusaidia kupunguza msongo wa mawazo. Hii ni kwa sababu menejimenti nzuri ya muda itakusaidia katika kukamilisha kila jambo kwa wakati husika hivyo kukuondolea wasiwasi na mawzo katika akili yako.

Itakusaidia katika kupiga hatua kimaendeleo. Hii ni kwa sababu menejimenti ya muda itakusaidia kuzingatia kufanya vitu vya msingi na ambavyo vinaweza kukusaidia katika kupiga hatua kimaendeleo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Pia unakuwa na nafasi nzuri ya kufikia malengo yako ya kimaisha. Hii ni kwa sababu menejimenti nzuri ya muda inakusaidia katika kufanya vitu kwa wakati, kwa umakini na ufanisi wa hali ya juu. Pia inakusaidia katika kutekeleza vipaumbele ulivyonavyo katika kufikia malengo yako ya kimaisha.

Hasara za kushindwa kutunza muda vizuri

Kushindwa kusimamia muda wako vizuri kutapelekea faida zilizotajwa hapo juu kugeuka na kuwa hasara.
Kwa mfano, kutakuwa na kukosekana kwa ufanisi katika kazi unayoifanya kutokana na ukweli kwamba ,unakosa umakini katika kile ambacho unakuwa unakifanya.
Pia itakupelekea kuwa na msongo mkubwa wa mawazo kwa sababu unakuwa unashindwa kukamilisha mambo yako kwa wakati unaotakiwa.

Mbinu za kutunza muda

Zifuatazo ni mbinu mbalimbali ambazo zitakusaidia katika kutumia muda wako vizuri.

Jiwekee malengo yako. Tafiti zinaonesha kwamba wale watu ambao wanajiwekea malengo wanakuwa na uwezo wa kuona ni kwa kiasi gani wametimiza kile ambacho walikidhamiria kukitimiza kuliko wale ambao hawana malengo.

Weka  vipaumbele vyako. Unaweza ukawa na vitu vingi sana vya kufanya kwa wakati mmoja, lakini unatakiwa kuzingatia kipaumbele chako katika hayo yote ni kipi hasa na kisha uanze na hiko.
Kwa mfano, unaweza ukawa unataka kusoma na kulala kwa wakati mmoja. Lakini unachotakiwa kufanya ni kuangalia ni kipi kati ya hivyo viwili ni kipaumbele chako wewe na kisha uanze nacho.
Hakikisha matendo yako yanaendana na kipaumbele chako. Kwa mfano, kipaumbele chako kilikuwa ni kutumia masaa mawili kwa ajili ya kusoma. Lakini wakati unasoma unaanza kutumia simu kwa kusoma ujumbe mbalimbali ambazo umetumiwa na hata kuzijibu, kitu ambacho kitakufanya upoteze muda wako na hata kupoteza umakini katika kusoma kwako.

Jifunze kusema hapana. Jifunze kukataa kufanya jambo ambalo unaona halina thamani yoyote katika maisha yako na wala haliendani na vipaumbele ulivyonavyo. Jifunze kukubali kufanya jambo ambalo lina thamani katika maisha yako kwa mfano, kufanya mazoezi, kukaa na familia yako, kupumzika na mengineyo yanayofanana na hayo.

Epuka kufanya vitu ambavyo vinakupotezea muda wako. Tambua vitu ambavyo vinakufanya upoteze muda kama vile meseji, mitandao ya kijamii, watu na vitu vingine. Ukishavigundua unatakiwa kuviondoa, usiruhusu muingiliano wa kitu chochote kile katika muda ambao unatakiwa kuzingatia jambo fulani.
Lakini pia jambo lingine ambalo linaweza kukufanya wewe upoteze muda ni pamoja na kuwa na mtazamo hasi katika jambo fulani. Hii ni kwa sababu unapokuwa na mtazamo hasi katika jambo fulani, utakuwa unakosa umakini katika jambo hilo na hivyo kukupotezea tu muda.
Usipoteze muda wako kulalamika kuhusu makosa ambayo umeshawahi kuyafanya hapo nyuma. Cha msingi unachotakiwa kukifanya ni kujifunza kutokana na makosa na kusonga mbele.
Usipoteze muda wako kujilaumu kuhusu makosa ambayo ulishayafanya kipindi cha nyuma, badala yake songa mbele.
Epuka kuwa na udhuru. Imezoeleka kuwa watu wengi hawapendi kufanya kazi mbalimbali ambazo huwa hawazipendi. Suluhisho pekee katika hili ni kufanya tu hizo kazi kwanza ili kuweza kuokoa muda.
Acha tabia za kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja. Unatakiwa kufanya jambo moja kwa wakati mmoja kwani kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kunaweza kukakupotezea muda wako.
Tafiti zinaonesha kuwa watu ambao wanadhani wanaokoa muda kwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja wanaweza wasikamilishe kwa haraka au kwa umakini kama ambavyo wangefanya kila jambo kwa wakati mmoja.
Kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja kunapunguza nguvu ya ubongo katika kufikiria lakini pia kunaleta msongo wa mawazo jambo ambalo linaathiri kumbukumbu katika ubongo. Wakati mwingine kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja ni jambo lisiloweza kuepukika, lakini hautakiwi kufanya hivyo kwa siku nzima.
Kama utazingatia jambo moja kwa wakati mmoja, utakuwa makini katika kile ambacho unakifanya  kwa wakati unaotakiwa.
Vilevile ukifanya jambo moja kwa wakati mmoja na kulimaliza kabla hujaenda kufanya jambo lingine, utajikuta unatumia muda mchache zaidi kulimaliza. Hii itakusaidia wewe kupata muda  zaidi wa kufanya kitu kingine ambacho ulipanga kukifanya.  
Hitimisho
Kwa ujumla, muda ni rasilimali ambayo inamilikiwa na kila mtu. Sote ni matajiri wa muda. Changamoto imo katika namna tunavyoutumia muda muda huo. Chunga muda wako.


MAHUSIANO

DALILI ZINAZOONESHA KUWA UPO KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI AMBAYO SIO SAHIHI  Sisi sote tunapenda kuwa na furaha pamoja na kupendwa  katik...